KADCO KUZILIPA FIDIA FAMILIA 429 KUFUATIA UPANUZI MKUBWA WA UWANJA....WENGINE WAAMBIWA WAVAMIZI - MUKAMAFUNNY BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 28, 2017

KADCO KUZILIPA FIDIA FAMILIA 429 KUFUATIA UPANUZI MKUBWA WA UWANJA....WENGINE WAAMBIWA WAVAMIZI




Kampuni ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kadco), inatarajia kulipa fidia ya Sh400 milioni kwa familia 429 zilizofanyiwa tathmini mwaka 2002 kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja.

Pia, wananchi hao watakaolipwa watatakiwa kuondoka eneo hilo kupisha upanuzi zaidi wa uwanja huo.

Hayo yalisemwa juzi na naibu waziri wa uchukuzi na mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Atashasta Nditiye wakati akizungumza na uongozi wa uwanja huo.

Alisema baada ya kutembelea uwanja huo na kuzungumza na uongozi, amebaini kuwapo kwa changamoto hiyo ya kulipwa fidia kwa wananchi hao ambao wamefanyiwa tathmini huku kukiwa na wananchi ambao hawakufanyiwa tathmini wakihitaji nao kulipwa.

Nditiye alisema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa watakaolipwa fidia ni wale waliofanyiwa tathmini mwaka 2002 ambao ni familia 429 tu, kwa wale walioongezeka baada ya tathmini hiyo ni wavamizi na hawatalipwa chochote.

“Tunaomba wananchi waelewe hilo, sisi tunalipa wale waliofanyiwa tathmini tu na idadi yao tunayo, Serikali inatafuta fedha kwa ajili familia hizo zitakapopatikana tutawalipa fidia zao,” alisema Nditiye na kuongeza:

“Kwa waliokuja baada ya tathmini hao ni wavamizi na hatutawalipa chochote, naomba waelewe hilo. Kumekuwapo na changamoto ya wananchi waliokuja baada ya tathmini kuhitaji nao kulipwa fidia jambo ambalo haliwezekani kabisa na Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya familia 429 tu si vinginevyo.’’

Alisema Serikali inataka kupanua uwanja huo na kujenga miradi mbalimbali, ikiwamo maduka na maeneo mbalimbali ya kupumzikia ili kuwawezesha wageni wanaofikia uwanjani hapo kupumzika badala ya kwenda mjini.

Naye mwenyekiti wa bodi ya uwanja wa Kia, Gregory Teu alisema kuwa, hivi sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hao waliofanyiwa tathmini, hivyo kuwataka ambao hawajafanyiwa tathmini kuondoka wenyewe kupisha shughuli za upanuzi wa uwanja huo.

Awali, akitoa taarifa kaimu mkurugenzi wa Kadco, Christopher Mukoma aliwataka wananchi hao kusikiliza maagizo ya Serikali inavyowaelekeza.

Mukoma alisema watakaolipwa ni wale waliofanyiwa tathmini tu, hivyo wengine kuanza kutafuta namna nyingine kabla shughuli za upanuzi wa uwanja huo hazijaanza.

Upanuzi wa Kia unatarajiwa kuongeza idadi ya abiria wanaotumia uwanja huo kufikia zaidi ya milioni moja na ndege 11 zinataweza kutua kwa wakati mmoja.

Pia, inaelezwa kuwa kufungwa kwa mashine za ukaguzi kusaidia kupunguza matukio ya upitishaji wa dawa za kulevya na utoroshaji wa nyara za Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages