MUHIMU KWA WENYE WATOTO:ZIFAHAMU SABABU ZINAZOWAFANYA WATOTO KUKOSA HAMU YA KULA - MUKAMAFUNNY BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 25, 2017

MUHIMU KWA WENYE WATOTO:ZIFAHAMU SABABU ZINAZOWAFANYA WATOTO KUKOSA HAMU YA KULA


Kukosa hamu ya kula ni tatizo la kawaida kwa watoto ambalo hupelekea wazazi wengi kuwa na wasiwasi juu ya afya ya watoto wao. Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha  kukosa hamu ya kula na tatizo hili linapojitokeza tunatakiwa kuwa watulivu na kujaribu kuchunguza kwa makini ni kwa nini mtoto anakosa hamu ya kula. Baadhi ya sababu zaweza kutatuliwa na mzazi au mlezi lakini sababu nyingine kama zisababishwazo na magonjwa zitahitaji msaada wa wataalam wa afya.

Moja ya sababu kubwa ambayo huwakosesha watoto hamu ya kula ni aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa kama Malaria, kuhara, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo humkosesha mtoto raha hupelekea watoto kukosa hamu ya kula.

Matatizo ya kifamilia na msongo ni sababu nyingine ambayo huwakosesha watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima watoto pia hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu wavipendavyo. Lakini pia watoto hukumbana pia na changamoto mbalimbali za kimaisha kama majukumu ya shule au pengine kukumbana na unyanyasaji kama kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao.

Kwa hiyo ili kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi hawana budi kuwa makini endapo wataona mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto. Kugundua na kuweza kuziondoa sababu zinazomsababishia mtoto msongo, tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea tena.

Lakini pia wakati mwingine hali hii hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalam kama Anorexia nervosa. Watoto wenye ugonjwa huu huweza kukaa muda mrefu bila kula ingawa hawana tatizo jingine, na endapo watapewa chakula huchagua aina fulani tu ya chakula jambo ambalo hupelekea kutopata mlo ulio kamili na hii hupelekea kupungua uzito pamoja na kudhoofu kwa afya zao .

Jambo hili linapojitokeza ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako kurejesha tena hamu ya kula.

Kiwango kidogo cha ukuaji wa mtoto huchangia  kupungua kwa hamu ya kula. Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, watoto hukua haraka lakini baada ya mwaka mmoja kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula wanachokula pia hupungua. Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida katika maisha ya watoto.

Sababu nyingine ambazo huchangia watoto kukosa hamu ya kula ni kama maudhi ya dawa, upungufu wa damu, uambukizi wa minyoo na matatizo ya mmeng'enyo mfano mtoto kutopata choo.

Maudhi ya dawa mbalimbali ambazo hutumika kutibu magonjwa kwa watoto yanaweza kuchangia watoto kukosa hamu ya kula. Mfano daktari akimwandikia mtoto dawa za antibiotiki, zaweza kusababisha tazizo la kukosa hamu ya kula. Kupoteza hamu ya kula kwa watoto wanaotumia antibiotiki ni maudhi ya dawa ambayo huwapata watoto wengi. Dawa nyingine pia zaweza kupelekea kupata maudhi ya dawa kama kichefuchefu na kutapika. Tatizo hili humalizika mtoto anapomaliza dawa na endapo atakuwa amepona.

Uambukizi wa minyoo huchangia tatizo hili. Minyoo huingia katika mfumo wa mmeng'enyo wa watoto na kusababisha upotevu wa damu. Minyoo hutegemea ufyonzaji wa damu kama chakula chao, na katika uambukizi sugu hupelekea kuvuja kwa damu,upungufu wa damu, kuhara, kichefuchefu, kutapika na kukosa hamu ya kula. Endapo mtoto ataonyesha dalili za umbukizi wa minyoo, ni vyema kuwaona wataalam wa afya ili kuweza kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu.

Ugonjwa wa upungufu wa damu ambao kwa kitaalam hujulikana kama anemia, husababishia watoto tatizo hili. Kiwango kidogo cha madini ya chuma katika damu, huwapata watoto ambao hawapati lishe ya kutosha yenye madini haya. Lakini pia anemia yaweza kusababishwa na uambukizi wa minyoo au hata magonjwa mengine. Watoto wenye anemia huwa wadhaifu na wasio wachangamfu, na kama ugonjwa usipotibiwa utaathiri afya ya mtoto hata maendeleo yake shuleni. Ni vyema mtoto akafanyiwa vipimo vya damu endapo utahisi au ataonyesha dalili za ugonjwa wa anemia.

Kwa watoto hasa wadogo, kukosa choo hupelekea kukosa hamu ya kula. Kwa hiyo inapotokea basi ni vyema kupata msaada wa wataalam ili mtoto aweze kuondokana na tatizo hilo.

Wazazi na walezi wazingatie yafuatayo ili kuboresha hamu ya kula ya watoto wao:

  • Kuwa na ratiba nzuri ya kumpa mtoto chakula, na mtoto apewa chakula anapokuwa na njaa.
  • Usiwagombeze au kutoa maonyo makali kwa watoto wakati wa kula.
  • Kuwa na milo midogo kati ya milo mikubwa.
  • Mpe mtoto kiasi kidogo cha chakula lakini mara nyingi kwa siku na siyo kumshindilia kwa wakati mmoja.
  • Usimlazimishe mtoto kula kama hana njaa.
  • Hakisha mtoto anashiriki katika michezo, kwa kuwa michezo huusisha matumizi ya nishati ya mwili na kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.
  • Wakati mwingine mpe nafasi mtoto wa uchaguzi wa chakula akipendacho, lakini chini ya uangalilizi wa mzazi au mlezi ili afanye uchaguzi ulio sahihi.
Wakati wote  wazazi na walezi tukumbuke kuwa tatizo la kukosa hamu ya kula ni la kawaida kwa watoto wengi, na tatizo linapojitokeza hatuhitajiki kuwa na wasiwasi kila wakati. Kama mtoto wako ana afya njema, anapata usingizi vizuri na ni mwenye furaha, hauna sababu ya kuwa na wasiwasi. Lakini kama tatizo litaendelea kwa muda mrefu, basi hatuna budi kuonana na wataalam wa afya kwa msaada zaidi.

1 comment:

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages