Siku moja baada ya kueleza kuwa mwili wake bado una risasi moja licha ya kutolewa nyingine 15, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema risasi hiyo ipo juu ya kiuno chini ya mfupa wa mgongo na kwamba ameelezwa na madaktari kuwa haiwezi kumletea shida yoyote.
“Ipo kwenye tishu sio kwenye mfupa wa mgongo. Hapo ilipo haina madhara yoyote. Kuiondoa kunahitaji ‘complicated operation’ ambayo ni ya hatari zaidi,” alisema Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alipozungumza na mwandishi wetu kwa simu jana.
Lissu amelazwa katika Hospitali ya Nairobi tangu Septemba 7 baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari mara baada ya kufika nje ya makazi yake mjini Dodoma na huenda akahamishiwa nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi.
Juzi jioni, katika mahojiano yake na kituo cha Televisheni cha Azam, mbunge huyo wa Singida Mashariki alizungumzia afya yake kwamba risasi 16 ziliingia mwilini mwake, saba zilitolewa na madaktari wa Nairobi na moja ipo mwilini mwake, licha ya kutoeleza iko sehemu gani.
Ufafanuzi wake huo wa juzi ulimaanisha kwamba risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya shambulio hilo alipofikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General) au hazikubakia mwilini baada ya kumdhuru.
Baada ya kueleza kuwa anaishi na risasi hiyo mwilini, mjadala uliibuka juu ya sehemu gani ya mwili ilipo risasi hiyo na gazeti hili kuamua kumtafuta ili kupata ufafanuzi wa kina.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema hana wasiwasi na mwili wake kuwa na risasi hiyo kwa sababu madaktari wamemhakikishia kuwa haiwezi kumletea madhara.
Alisisitiza kuwa kutokana na hali hiyo, ameelezwa kuwa kuiondoa kunaweza kuwa hatari zaidi.
Akizungumzia suala hilo, daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya fahamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Bashir Nyangasa alisema wapo watu wengi wanaioshi na risasi mwilini.
Alibainisha kuwa madhara yanaweza kutokea kama risasi itakuwa katika mshipa wa damu au wa fahamu.
“Risasi ikiwa katika mshipa wa damu inasababisha damu isiweze kutoka chini kwenda juu na inapokuwa katika mshipa wa fahamu inakandamiza na kusababisha maumivu lakini ikiwa sehemu ya misuli haina madhara,” alisema Dk Nyangasa na kuongeza, “Ikitokea ukapata jipu (sehemu iliyopo risasi) inakuwa rahisi kuitoa kwani itatoka wakati usaha unatoka, ikiwa imekaa sehemu tofauti na mishipa ya damu na fahamu, hakuna madhara unaishi vizuri kabisa.”
Katika ufafanuzi wake wakati wa mahojiano na Azam, Lissu alieleza jinsi alivyopigwa risasi hizo zilizompata sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo mikononi.
Huku akionyesha mkono wake wa kulia alisema, “Nilipigwa risasi hapa, upande huu na ikatokea hapa. Madaktari wanasema kwamba ilichakaza kabisa mfupa ilikopita, hakukuwa na mfupa. Ilibidi waungeunge kwa hiyo kuna chuma kinachounganisha mfupa wa huko mbele na nyuma kwenye mkono huu.”
#Mwananchi

No comments:
Post a Comment