DKT SHEIN AKUTANA NA BALOZI WA COMORO HAPA NCHINI....AAHIDI KUENDELEZA UHUSIANO WA KISTORIA KATI YA NCHI HIZI MBILI - MUKAMAFUNNY BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 7, 2018

DKT SHEIN AKUTANA NA BALOZI WA COMORO HAPA NCHINI....AAHIDI KUENDELEZA UHUSIANO WA KISTORIA KATI YA NCHI HIZI MBILI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na visiwa vya Comoro hasa katika kukuza mila na utamaduni ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano kati ya pande mbili hizo.

Akizungumza na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Mohammed Fakih Al Baadawy aliyefika Ikulu mjini Zanzibar, Rais Dk. Shein alimuahidi Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo ambao ulitiwa nguvu zaidi baada ya kusainiwa Mkataba wa Makubaliano mnamo mwaka 2014, wakati alipofanya ziara nchini humo.

Mbali ya uhusiano wa kimaendeleo kati ya Zanzibar na Comoro, Dk. Shein alisema kuwa nchi mbili hizo zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu katika kukuza mila na tamaduni sambamba na mafunzo hasa katika elimu ya dini ya Kiislamu

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar itashiriki kikamilifu katika Kongamano la kimataifa juu ya maisha ya Marehemu Sheikh Sayyid Omar Abdallah, maarufu Sheikh Mwinyi Baraka litakalofanyika mjini Moroni, Comoro kuanzia April 03 hadi 06, 2018.

Rais Dk. Shein aliyapongeza malengo ya Kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha vijana juu ya masuala muhimu aliyoyahubiri Sheikh Mwinyi Baraka na kusisitiza kuwa kwa upande wa Zanzibar wapo wanaomfahamu wakiwemo walimu na wanazuoni wa zamani ambapo wapo baadhi yao ambao wako hai hivyo, ushiriki wa Zanzibar ni muhimu katika Kongamano hilo.

Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamni sana ushirikiano na uhusiano uliopo kati yake na Comoro katika sekta ya elimu, hasa elimu ya Dini ya Kiislamu ambapo wananchi waliowengi wa Visiwa vya Comoro waliipata elimu hiyo hapa Zanzibar na kwenda kuifanyia kazi katika nchi hiyo.

Aliongeza kuwa Masheikh, Wanazuoni, na Maulamaa kama vile kina Sheikh Mwinyi Baraka waliweza kufanya vyema katika kuhakikisha wanakuwa Mabalozi wazuri na kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya elimu ya dini ya Kiislamu hivyo, ni vyema wakakumbukwa kwa juhudi zao hizo.

Hivyo, Rais Dk. Shein alikubaliana na kupongeza wazo la Balozi huyo wa Comoro katika Ushirikiano wa Vyuo Vikuu vya nchi hizo kikiwemo chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA ) na Chuo Kikuu cha Comoro katika maandalizi ya Kongamano hilo la Kimataifa ambalo litazidi kutoa mwanga wa ushirikiano katika sekta ya elimu.

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza ushiriki wa Zanzibar katika Kongamano hilo pamoja na kuunga mkono wazo la kuwepo kwa Makumbusho maalum ya Sheikh Mwinyi Baraka nchini Comoro ambapo akiwa katika ziara yake nchini humo mwaka 2014 alizuru kaburi la Sheikh huyo.

Nae Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Mohammed Fakih Al Baadawy alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Comoro na Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya nchi mbili hizo pamoja na watu wake ambao wana udugu wa kihistoria.

Balozi Al Baadawy alimueleza Dk. Shein kuwa Comoro itaendeleza na kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo hasa katika sekta mbali mbali za maendeleo na zile za kijamii kwa kutambua udugu wa damu uliopo kwa watu wa nchi mbili hizo.

Aidha, Balozi huyo alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza vyema uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ambapo suala la Mila na Utamaduni lilihusishwa na limekuwa likifanyiwa kazi vyema na kuanza kuzaa matunda.

Hivyo, Balozi huyo wa Comoro alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Shein azma ya nchi yake kufanya Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya kumuenzi Sheikh Mwinyi Baraka, ikiwa ni miaka 100 ya kifo chake sambamba na kumuelezea Sheikh huyo ili azidi kufahamika na vizazi vilivyopo na vijavyo wakiwemo vijana, ili waweze kuutambua mchango wake.

Alieleza kuwa ushiriki wa Chuo Kikuu cha SUZA katika kongamano hilo ni muhimu sana na utasaidia kupata mambo mengi muhimu kutoka kwa wasomi wa chuoni hapo pamoja na wadau wengine ikiwemo Taasisi ya Mwinyi Baraka ya Zanzibar huku akieleza ushiriki wa wadau wengine kutoka Marekani, Uengereza, Ufaransa, Ujerumani na sehemu nyengine duniani.

Alisisitiza kuwa Sheikh Mwinyi Baraka alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza elimu hasa elimu ya dini ya Kiislamu ambapo mbali ya elimu ya dini ya Kiislamu pia, alibobea katika elimu ya dunia ambapo alisoma vyuo mbali mbali duniani na kupata Shahada ikiwemo Chuo Kikuu cha Makerere Uganda, Oxford cha Uingereza na Vyuo vyengine vya nchi za Kiarabu.

Sheikh Mwinyi Baraka alizaliwa Zanzibar mnamo mwaka 1918 na kufariki Comoro mwaka 1988 ambaye alikuwa msomi na mwanachuoni mashuhuri ambapo Kongamano hilo la kwanza la Kimataifa litaweza kuhamasisha na kuelimisha watu juu ya safari na sifa za Sheikh huyo ambaye alikuwa mwalimu, mbunge, mwanadiplomasia, mhadhiri, mwanasayansi, mwanasheria na msomi wa dini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages