RAIS MAGUFULI: TEMBEENI KIFUA MBELE......SERIKALI HAIJALALA NA KAMWE HAITALALA - MUKAMAFUNNY BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 3, 2018

RAIS MAGUFULI: TEMBEENI KIFUA MBELE......SERIKALI HAIJALALA NA KAMWE HAITALALA


Rais John Magufuli amezindua rada nne za kiraia za kuongozea ndege huku akisisitiza kuwa serikali yake haijalala na kamwe haitalala katika kuwatumikia Watanzania wanyonge pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaopinga juhudi hizo. Rada hizo nne zitatumika katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Songwe na Zanzibar.

Rais Magufuli alisema, serikali imekuwa ikijikita katika kuwasaidia wananchi wake kwa hali na mali lakini wapo watu wachache wanaobeza harakati hizo lakini akasema hawatafanikiwa.

Alisema, katika kuidhinisha kuwa serikali haijalala, imekuwa makini katika kuwahudumia wananchi wake kwa kuwajengea misingi mizuri ya uchumi.

Alisema; “Nimeshangazwa na masuala sijui ya waraka, sijui nini ninachotaka mfahamu ni kuwa wapo watu ambao wanaonea wivu maendeleo yetu haya, kwa sasa nchi ipo vema na ina uchumi mzuri na kamwe serikali ninayoiongoza mimi hailali na wala haitalala.”
Kuhusiana na rada hizo Rais Magufuli alisema pamoja na kutumika katika kuongozea ndege lakini pia zitatumika katika kuimarisha usalama wa nchi.
Alisema, ni hatari na aibu kwa nchi kubwa kama Tanzania ndege zinazoingia nchini kuendelea kuongozwa na rada za Kenya, huku kukiwa na mapato yanayopotea kutokana na hali hiyo. Rais Magufuli alisema Tanzania mpaka wakati huu ina rada moja tu ya kiraia ambayo inatumika kuongozea ndege.

Alisema rada hiyo ambayo ipo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ina uwezo wa kuhudumia asilimia 25 tu ya anga la Tanzania. Rada hiyo ilinunuliwa mwaka 2002 ikitarajiwa kutumika kwa miaka 12, imepungua uwezo wake kutokana na uchakavu.
Alisema kutokana na hali hiyo mashirika makubwa ya kimataifa ya ndege yanasita kufanya safari zake nchini na kuinyima nchi fedha nyingi.
Rais Magufuli alisema amefurahishwa na mradi huo kwa kuwa ukikamilika Tanzania itakuwa na uwezo wa kuliona anga lake lote.
Alisema kukamilika kwa mradi huo pia kutasaidia kuliona anga la nchi jirani hususani Burundi na Rwanda ambazo Tanzania imekasimiwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Alisema hatua hiyo itaimarisha anga la Tanzania lakini zaidi ya hapo mradi huo utakapokamilika utarahisisha shughuli za uongozaji wa ndege na kuiongezea mapato nchi.
“Hivi sasa tumekuwa tukipoteza tozo za kuongezea ndege takribani shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka kutokana na ICAO kukasimu sehemu ya anga la Tanzania kwa nchi jirani ya Kenya,” alisema Rais Magufuli.
Alisema ana uhakika mradi huo ukikamilika sehemu hiyo ya anga itarejeshwa na hatimaye Tanzania kuongoza na kulinda anga lake lote yenyewe.
Mradi huo umegharimu Sh bilioni 67.3 na zote zimelipwa na serikali ya Tanzania. Alisema usafiri wa anga ni muhimu katika biashara na ukuaji wa Sekta ya Utalii kwa sababu katika sekta hiyo duniani zaidi ya asilimia 70 inategemea usafiri wa anga.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika Sekta ya Utalii duniani hivyo Sekta ya Usafiri wa Anga itaongeza idadi ya watalii watakaokuja nchini kutoka milioni tatu ya sasa hadi milioni tano. Kutokana na ukweli huo, Rais Magufuli alisema uimarishaji na uboreshaji wa usafiri wa anga haukwepeki.
Alisema kutokana na ukweli huo Serikali ya Tanzania imepanga kununua ndege sita ambapo tatu tayari zimetua na zingine zitatua ndani ya mwaka huu.
Awali Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.
Alisema mradi huu ambao utatekelezwa kwa miezi 18 hadi kukamilika, ulitiwa saini mwaka jana na utekelezaji wake ulianza mwaka huohuo huku kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya Ufaransa.
Alisema mkakati uliowekwa na wizara yake ni kukifanya Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kuwa njia panda ya biashara kwa mataifa mbalimbali.
Aliipongeza TCAA kwa kugharamia asilimia 45 ya fedha za mradi mzima huku asilimia 55 ikigharamiwa na serikali kuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema, rada hizo nne zikifungwa TCAA inaongeza pato lake la ndani kutokana na tozo itakayokuwa ikipata.
Alisema, kwa kuwa rada hizo zitakuwa na uwezo wa kuongeza ndege nyingi zaidi hivyo pato linalotokana na tozo hizo litaongezeka ambapo alisema, kwa tozo la Dola za Marekani 300 rada moja inaweza kuongoza ndege nane kwa saa moja tofauti na kwa sasa ambapo inaongoza ndege mbili kwa saa.
Alisema, fedha hizo zote za mradi zitahusisha taasisi za serikali katika utekelezwaji wake ambapo miamala itafanyika kupitia Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), mawasiliano yote yatasimamiwa na Shirika la Mawasiliano ya Simu (TTCL) huku Wakala wa Ujenzi Tanzania nayo itahusika kwa ukaribu katika ushauri.
Alisema, tayari wataalamu 33 kutokea TCAA wapo nchini Ufaransa wakifundishwa masuala ya utaalamu wa kutumia rada hizo, na kuwa mradi mzima utahusisha ujenzi wa majengo, uzio, barabara za kwenda kwenye eneo la rada zitakapofanya kazi pamoja na mafunzo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages