Mapema siku ya leo Jumapili Januari 14, 2018, Rais John Magufuli amekutana na Rais Paul Kagame wa Rwanda na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao ambayo yamerushwa mubashara (live) na vituo vya Televisheni nchini, Marais hao wamekubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Marais hao wamekubaliana kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Isaka Kahama hadi mji wa Kigali nchini Rwanda, na kusema jiwe la msingi la ujenzi huo kuwekwa kabla ya mwezi Desemba mwaka huu.
“Tumekubaliana na Rais Kagame kujenga reli kutoka Isaka, Tanzania hadi Kigali, Rwanda, na tumewaambia mawaziri wa nchi hizi mbili wakutane mapema ili kujadili uwezeshaji wa mradi huu, upembuzi yakinifu umeshafanyika” amesema Rais Magufuli.
Marais hao wamezungumzia pia suala la wananchi wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara pamoja ili kukuza uchumi wa nchi zao.
Suala la ajira kwa vijana pia limepewa kipaumbele katika mazungumzo ya leo, ambapo Rais Kagame amekiri kuwa hii ni changamoto kubwa kwa bara la Afrika, na kutaka kila nchi kuchukua hatua ili kutatua changamoto hii.
“Tatizo la Ajira kwa vijana katika Afrika ni tatizo la Jumla, na linahitaji kila nchi kuchukua hatua kuhakikisha inajenga hatma ya vijana” amesema Rais Kagame.
Kwa upande wake Rais Magufuli amewataka Vijana kujifunza kupenda kazi, na kusema hakuna kitu cha bure hivyo vijana waache kuwa na mawazo ya kukimbilia nchi za ulaya kwenda kutafuta kazi na badala yake watafute njia za kutatua changamoto hii wakiwa ndani ya nchi.
“Vijana tujifunze kupenda kazi, hakuna cha bure, tusiwe na mawazo kukimbilia Ulaya kuwa ndio kupata solution” amesema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine Rais Mgufuli amempongeza Rais Kagame kwakusema ni mwanamapinduzi wa kweli wa Kiafrika na kuwa Tanzania inamuunga mkono katika katika nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais Kagame amehaidi kuendelea kutembelea nchi ya Tanzania kwaajili ya kupata ushauri juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo kwa nchi hizi mbili.
No comments:
Post a Comment