SERIKALI HAITASITISHA MKATABA WA KAMPUNI YA CHAI MARUKU - MUKAMAFUNNY BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 4, 2018

SERIKALI HAITASITISHA MKATABA WA KAMPUNI YA CHAI MARUKU


Related image
Serikali imesema kuwa haitasitisha mkataba na Mwekezaji wa Kampuni ya Chai Maruku, iliyoko mkoani Kagera, kwa sababu mgogoro wa malipo uliopo baina ya  kampuni hiyo na wakulima pamoja na wafanyakazi wake unaelekea kutatuliwa.

Hayo yameelezwa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Jason Rweikiza (CCM), aliyetaka kujua sababu za Serikali kutovunja mkataba na mwekezaji huyo na kurejesha umiliki kwa Serikali au kwa mwekezaji mwingine atakayejali maslahi ya wakulima na wafanyakazi.

Katika swali lake la msingi, Mhe.   Rweikiza alisema kuwa tangu Kampuni hiyo ibinafsishwe kwa mwekezaji, kumekuwa na malalamiko ya wakulima kutolipwa  fedha za mauzo ya chai kwa wakati na wafanyakazi kutolipwa  mishahara na stahiki zao ipasavyo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, katika kutatua mgogoro huo Serikali kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utendaji na uendeshaji wa Kampuni hiyo kwa kufanya vikao kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai (TASHTIDA).

Alisema kuwa katika vikao hivyo haki ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala la haki za wafanyakazi pamoja na madai ya wakulima, ambapo mpaka sasa mwekezaji amekubali kulipa madai ya wakulima kiasi cha Sh. milioni 12 huku wakiendelea kujadili namna ya kutatua suala la madai ya wafanyakazi.

Dkt. Kijaji aliahidi kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha haki za wakulima na wafanyakazi hazipotei.

Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa  Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
4/4/2018

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

Pages